Je, Wewe Ni Mwaminifu Kwa Kiasi Gani?

Tazama wapendezwa na kweli iliyo moyoni” (Zaburi 51:6).

Uaminifu ni maadili ya ukweli katika kufungamana na mambo yote ya maisha. Kwa hakika uaminifu ni jambo la moyoni, pia ni fundisho la msingi la Injili ya Yesu Kristo. Mungu anajua mawazo na makusudi ya moyo. Anatambua ukweli kama msingi muhimu kwa maana yeye ni Mungu wa ukweli. (Kumb. 32:4) Hakika atabariki uaminifu uliokamilika wa moyo wetu.

Je, unao tabia ya kusema ukweli wakati ungeweza kupatikana na jambo, lakini ukawa si mwaminifu wakati ambao hakuna atakayekugundua?

Je, kwa makusudi unaweza kumridhisha mtu kwa ushawishi usio wa kweli?

Je, unaweza kufanya manunuzi kwa kukopa wakati ulifahamu kwamba huna uwezo wa kulipa?

Je, unamwambia Mungu jinsi mambo yalivyo wakati unapomwomba?

Je, kwa uaminifu unalitenda kila jambo ambalo unafahamu Mungu anakutaka ulitende?

Maandiko kamili ya: Je, Wewe Ni Mwaminifu Kwa Kiasi Gani?

Je, wewe ni mwaminifu kuhusu mafundisho ya Biblia?

Je, jinsi unavyojifanya kuonekana, kweli ndivyo ulivyo?

Kuna hadithi ya kuchochea hisia katika Agano Jipya ya mtu aitwaye Anania na mkewe Safira katika kitabu cha Matendo 5:1-11. Waliuza mali yao kama wengine nao walivyofanya na kujifanya kutoa fungu lote kwa kanisa, wakati kwa hila walikubaliana kubakiza sehemu ya malipo kwa ajili yao. Anania na Safira walileta pesa hizi mbele ya viongozi wa kanisa wakisema kwamba waliuza shamba hilo kwa kiasi hicho walicholeta. Udanganyifu wao ulihukumiwa na Mungu mara moja na kuadhibishwa kwa kifo. Katika habari hii ya kanisa la mwanzo, unafiki (au udanganyifu) ulikuwa ukiadhibishwa kwa ukali. Mungu hapuuzi uzushi huu. Nasi kama Anania na Safira huenda tunaweza tukatoa uzushi unaoridhisha hata kama maneno tuyasemayo siyo ya uongo. Twaelekea kusahau uwajibikaji wetu mbele za Mungu. Mungu ajua jinsi mioyo yetu ilivyo, na anatutegemea tuwe waaminifu na wa kwelikweli.

Mnafiki hujifanya kuwa mtu ambaye siye yeye. Huenda anadai kuwa mwaminifu, lakini wakati ambao ingekuwa manufaa kwake, yuko tayari kusema uongo. Labda anaweza kuzungumzia vizuri kuhusu mahitaji ya wasiobahatika, lakini siye mkarimu wa kutoa muda wala msaada wakati maafa au matatizo yakitokea. Mtu mwingine aweza kujifanya kuwa mkarimu kujishughulisha na mambo ya majirani zake, na bado akatumia fursa hio kuwasengenya. Mwingine huenda anajionyesha kuwa mtu mnyofu, lakini bado yuko tayari kuchukua pesa za mtu mwingine, maadamu asigunduliwe katika tendo hilo. Huenda atajaribu kujiaminisha binafsi  kwamba anaishi maisha ya juu kitabia kuliko watu wengine wakati yeye ni mdanganyifu. Mtu aliye na tabia hizi ni mnafiki wala si mwaminifu.

Unafiki wa wanadamu kila wakati ni kitu cha kumhuzunisha Mungu. Yesu asema, “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami” (Mathayo 15:8). Changamoto kubwa kwa mwanadamu ni kuweka mdomo na moyo kwa pamoja. Uaminifu kutoka ndani yetu ndio ufunguo wa kupata neema na fadhili kwa Bwana.

Mkristo wa kweli ni mfano wa uaminifu. Kustawi kwake kiroho huendana na unyofu wake mbele ya Mungu. Uaminifu kwa binadamu wenzetu pia ni muhimu na unahitaji usikivu wa umakini. Katika maneno yetu, matendo ya shughuli zetu, na hata makubaliano ya kibiashara ni lazima tuhifadhi imani kwa watu wote. Ili tutende hili, ni lazima tuwe tayari kupata hasara kwa ajili ya ukweli.

Kuna somo tunaloweza kujifunza kutokana na simulizi hii. Mwalimu alimwuliza kijana mmoja swali:

“Je, ungesema uongo ukilipwa shilingi 50?”

“La hasha, mama” kijana akamjibu.

“Je, ungeweza kusema uongo ukilipwa shilingi elfu mbili?”

“La hasha, mama” kijana akamjibu.

“Je, ungeweza kusema uongo ukilipwa shilingi milioni mbili?”

“Lo!” akajisemea moyoni. “Ni kitu gani nisichoweza kukifanya nikiwa na shilingi milioni mbili?”

Wakati akisitasita, kijana mwingine nyuma yake akasema, “La hasha, mama”.

“Ni kwa nini?” mwalimu akauliza.

“Kwa sababu uongo unashikamana na mtu. Wakati hio hela zitakapoisha, na vitu vyote vizuri vilivyonunuliwa na pesa hizo vimetoweka, UONGO utabakia pale pale ulipo.”

Ukweli una umuhimu kiasi kwamba tungekuwa tayari kusumbukiwa kwa ajili yake. Sisi tukiwa tayari kusema uongo ili tujiokoe kutoka kwa kuaibishwa kwa muda mfupi, ni gharama kubwa mno kulipa kwa ajili ya kupotewa na uadilifu wetu. Pesa zipatikanazo kwa njia ya ujanja ni malipo duni kwa kujipatia dhamiri iliyonajisika, na hukumu ya milele ya Mungu inayokuja.

Je, wasema kwamba unatembea katika nuru ya Mungu na wakati huo huo unayatenda matendo maovu kama:

  • Unakataa kumsamehe ndugu au dada yako?
  • Hufanyi mapatano unapomtendea mtu vibaya?
  • Unatia chumvi kwenye ukweli?
  • Unavunja ahadi zako?
  • Unamwibia Mungu sadaka na zaka zake?
     

Uaminifu ni mtihani wa moyo. Mungu anafahamu mioyo yetu, na hakuna kitu kilichositirika kwake. Walakini wakati mwingine hatuwezi kumwambia Mungu kwa kadiri anavyotujua na jinsi tunavyojihisi ndani mwetu. Huenda hatuwaonyeshi jinsi ndivyo tulivyo kwa watu wengine. Mtu wa kweli mwenye furaha ni yule aliye mwaminifu mbele za Mungu, na anajikubali na kukiri jinsi alivyo. Na tukifungua mioyo na maisha yetu kwa Mungu, matatizo haya yote yanatatuliwa.

Malengo na misimamo yetu yanahitaji kuwasilishwa kwenye kipimo cha uaminifu. Kufaulu mtihani huu katika matendo yetu kwa Mungu na wanadamu, twahitaji mabadiliko ya ndani ya moyo, kwa maana mambo ya nje yanafafanua utu wetu wa ndani. Je, wewe ni mwaminifu? Mungu anatudai unyofu, watu wengine wote wanautegemea, na sisi wenyewe tutanufaika kwa kuushika. Ndiyo maisha yaliyo na thamani. “Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia.” (Waebrania 13:18 Tafsiri la NENO). Soma pia Mambo ya Walawi 19:35-36 na Mithali 19:5.

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Nguvu Za Giza

Kutambua Mbinu za Shetani kwa Kutumia Mwanga wa Neno la Mungu.

Lengo la Biblia Takatifu silo kuangalia hasa Shetani na kazi zake. Japokuwa tunapata mengi kwenye Biblia yanayofunua tabia zake na kazi zake.

Wakati fulani Shetani alikuwa malaika, lakini aligeuka kinyume cha Mungu, Muumba wake, na akatamani kuwa kama Mungu. Matendo ya ufalme wa giza wa Shetani siyo mageni. Yanaonyesha dhahiri jitihada za Shetani kwa miaka kupingana na Ufalme wa Mungu. Anatoa mbadala wa kile ambacho Mungu anatimiliza kwa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu.

Twasoma katika kitabu cha Kutoka juu ya nguvu ya walozi wa Misri waliojaribu kufanya miujiza Mungu aliyofanya kwa mkono wa Musa. Na kwenye kitabu cha Ayubu, Shetani anadhihirishwa kama mwenye wivu sana juu ya uaminifu wa Ayubu kwake Mungu. Alitumia ukatili na unyang’anyi ili ajaribu kumlazimisha Ayubu kwenda kinyume na Mungu.

Njia za shetani zinatambuliwa na: Woga, vitisho, ahadi za kupata anasa na nguvu, misukumo, mashaka, na tuhuma. Baadhi ya mambo ya kwanza anayoyatambulisha kwetu yanaonekana ni ya kuvutia sana na ya kusisimua. Anashauri, “Ungependa kujua mambo ya mbeleni au kuwa na ufahamu ambao wengine hawawezi kuwa nao?” Anaweza kukupa uponyaji ambao uko nje ya idara ya kisayansi. Utabiri wa mambo yajayo huenda unaonekana kwamba hauna madhara wala ubaya, lakini unafuatwa na mengine ya uchawi wa macho, pamoja na kutumia dawa za kienyeji na uchawi wa kumroga mtu, na hatimaye kumpelekea mautini. Wazo linaanza kutuingilia kuwa kuna baadhi ya roho za kuheshimiwa na kuogopwa kwa sababu ya nguvu zilizo nazo juu yetu. Kwa hiyo, Shetani anawanasa hao wasiokuwa waangalifu kwenye mtego wake wa kuendeshwa na woga kwake na roho zake.

Watu wengi sana wamekamatwa na shauku ya vitu ambavyo, kwa mara ya kwanza vilionekana kuwa vyema. Kwa kufanya majaribio ya utabiri wa mambo yajayo na uchawi wa aina mbalimbali, watu wanajiweka kwenye mazingira hatarishi ya kusumbuliwa zaidi na mapepo ya giza.

Lengo la shetani ni kumomonyoa na hatimaye kuharibu imani ya mkristo kwa Mungu. Mkristo apata ushindi kwa kuwa na imani kwa Yesu Kristo peke yake. Wakati mwingine hamu ya kujua visivyojulikana au matamanio ya nguvu vinamsukuma mtu afanye majaribio na hayo ambayo ni ya ufalme wa Shetani. Imani ya kukaza kwa Mungu humpumzisha mtu asivutiwe na yale yasiyojulikana na pia inamimarisha kabisa katika nguvu za Kristo.

Maandiko kamili ya: Nguvu Za Giza

Yale yaliyoanza kutokana na shauku au majaribio punde yanamnasa mtu kwenye wavu wa hofu, hofu ya kile kinachoweza kutokea mbeleni, hofu ya nguvu kuu, hofu ya watu wengine, hofu ya Shetani mwenyewe. Hizi hofu zinamfunga mtu aliyeruhusu mwenyewe kujihusisha na matendo yasiyo na uhakika. Kutibu hofu hii, Shetani anadai kuwa anao dawa nzuri: Eti atatoa nguvu zaidi kama mtu atajisalimishia utaratibu fulani au kutii amri kadhaa. Shetani asema kwamba hofu ya roho nyingine zinaweza zikashindwa kwa kujipatia nguvu kubwa zaidi kwetu wenyewe. Kwa hiyo mtu anaingizwa kwenye hatua za kufikia nguvu zaidi ambazo, badala ya kumpandisha kwenye kiwango cha juu cha amani, zinamzamisha chini katika kina kirefu cha machukizo ya kishetani. Usalama ulioahidiwa na shetani hauonekani, na hubadilishwa kwa uhitaji wa kulindwa na nguvu zilizo juu zaidi kwenye huu ufalme wa uovu. Huu ndio mfumo wa kishetani.

Mpango wa shetani ni kumzidi Mungu. Shetani aliumbwa kuabudu, na sio kuabudiwa. Yeye sio nguvu ya juu; hawezi kumzidi Mwana Kondoo wa Mungu; hawezi kutoa amani; hana nia na ushindi wetu. Hata hivyo anaendelea na kazi ya kuwatawala watu ili watu wamtumikie yeye. Anajaribu kuleta mashaka kuhusu Mungu na ufalme wake. Anajitahidi kuanzisha taasisi yake na yeye akiwa kama mfalme. Hii inaendelezwa kwa utaratibu wa hofu na udanganyifu wa nguvu. Anafanya miujiza ili awashangaze na kushawishi watu kusudi awawekee kifungo akilini mwao (2Wakorintho 11:14,15). Madhara ya mtego huu ni kuharibu amani na usalama kwa watu binafsi, majumbani, na hata serikalini. Hio inawakamata watu, na inasababisha wajisikie kutishwa sana kama watajaribu kutorokea ufalme huo.

Shetani ni mkali sana, mchoyo sana, mkatili sana, adui mbaya sana uliye naye wewe. Yeye hana heshima hata kidogo. Yeye ni mwongo. Hakuna ukweli ndani yake- “Yeye ni mwongo, na ni baba wa huo [uongo]” (Yohana 8:44). Yeye ni muuaji, mharibifu. Yeye ni mfano wa chuki na uovu. Yeye ni mwovu kabisa ambaye hana uzuri uliobakia kwake!

Shetani ni mchochezi wa maovu yote. Hakuna kosa wala dhambi ambayo kwake ni ovu sana au chafu sana kwake. Yeye ni chanzo cha chuki zote, mauaji yote, kila aina ya kutesa watoto au kupiga wanawake, kila aina ya madawa ya kulevya, kila aina ya uzinzi, ndoa zote zilizovunjika, kila aina ya kutokuelewana, kila uchawi, kila kutokuwa na uaminifu. Anafurahi kusababisha hamu ya kuvunja sheria na uovu, uvunjaji wa sheria unaofanyika juu ya watu wengine wema ambao, kwa bahati mbaya, wanaangukia mikononi mwa wasio haki na wapotovu. Yeye ni mkatili na hana msamaha. Hana huruma kwa hao wanaopata mateso. Kumwaga damu na vifo ndio silaha anazotumia kutekeleza kazi zake. Amekuja “kuiba, kuua, na kuharibu” (Yohana 10:10).

Mwisho wa milele wa Shetani ulishaamulika. Kuna sehemu ya moto wa milele ilishaandaliwa kwa ajili yake na malaika wake (Mathayo 25:41). Anajishughulisha na kupata watu wengi kadiri atakavyoweza ili wapate hayo mateso pamoja naye. Anajua anaweza kufanya hivi kwa kuimomonyosha, kuidhoofisha, na mwishowe kuiangamiza imani yetu kwa Mungu. Atafanya hivi kwa kulipinga Neno la Mungu kwa uwazi, ama kwa ujanja na werevu anawahamasisha “wakristo” walio vugu vugu, wasiojali, na waliokubali Ukristo usio na masharti.

Kuna ukombozi kutoka kwenye umiliki na utumwa wa Shetani. Atakufanya uamini ya kuwa hakuna njia ya kutoka. Biblia inatuambia ya kwamba Yesu alikuja kuwaweka huru waliotekwa mateka. Amekuja kuleta uzima. Yesu ni njia, kweli, na uzima (Yohana 14:6). Wakati alipokuwa hapa duniani, Yesu alionyesha nguvu zake juu ya Shetani kwa kushindana na majaribu ya Shetani na akitupa nje nguvu za giza kwa kutumia Neno la Mungu (Mathayo 4:1-11; Marko 9:25,26). Yesu alishinda nguvu za Shetani kwa kifo chake msalabani na kufufuka kwake kutoka wafu.

Je, tunawezaje kujumuishwa katika ushindi huo wa kumzidi huyu adui mkuu wa nafsi zetu? Kwanza, lazima tufahamu ya kwamba tulikuwa tumetekwa na shetani na kufungwa na hofu yake. Lazima tukubali kwamba huku ni hali ya dhambi na kwamba tumepotea tukibakia hali hii. Tunapogundua hili kwamba hatuwezi kujiokoa wenyewe kutoka mkononi mwa Shetani, lazima tumlilie Mungu ukombozi wake kwa moyo wetu wote. Lazima tuzitubu na kuziacha dhambi zetu. Twahitaji kukubali kwa imani, damu ya Yesu Kristo yenye utakaso kwa ajili ya dhambi zetu. Lazima tujitoe nafsi zetu kwa Mungu, kukubali msamaha wake na kwa uaminifu kutii Neno lake. Tunapotimiza haya masharti, anatupa amani kwake, anayatuliza mahangaiko mioyoni mwetu, anasamehe dhambi zetu, anatufanya kuwa kiumbe kipya na kutufanya mmoja wa wanawe. Hii ndio inamaanisha kuzaliwa upya. Yeyote anayepinga mwito wa Mungu bado yumo katika ufalme wa Shetani, na mwishowe, mdanganyi atampeleka huyo mtu pamoja naye kwenye mateso ya milele.

Kama huelewi mpango ambao Mungu amekuwekea, jifunze Neno la Mungu, na umwombe Yeye kwa uaminifu moyoni, na atakuonyesha njia. Mungu anakuita kwake na anataka wewe utoroke na utumwa wa Shetani. Mungu akubariki. Soma Zaburi 91.

Masomo Mengine:

Luka 11:20-23 Mmoja mwenye nguvu zaidi ya Shetani

Warumi 6:20-23 Kuwa huru kutoka kwenye dhambi

Isaya 61:1 Kuwekwa huru mateka

Warumi 8:1,2 Kuwa huru na laana na hatia

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Yesu Kristo Atakuja Tena

Bwana Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wanadamu kutoka kwa dhambi zao. “Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa akawa ana mfano wa wanadamu” (Wafilipi 2:7). Alikufa kwa ajili ya dhambi za watu wote ulimwenguni, alizikwa  na akafufuka tena (1Wakorintho 15:4), kisha akapaa kwenda mbinguni tena (Matendo 1:9). Mitume walimwona na pia waumini zaidi ya mia tano, baada ya kufufuka. Baada ya kupaa kwenda mbinguni, malaika wawili waliwaambia mitume kwamba kurudi kwake kutafanana na kupaa kwake. Ni Mungu tu ndiye anayefahamu ni lini Bwana atarudi. Huenda itakuwa ni jioni au usiku wa manane, au wakati wa asubuhi au alasiri. (Marko 13:35) “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja” (Mathayo 24:44).

Baadhi wametabiri wakati wa kurudi kwake, hadi siku na saa. “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila baba peke yake” (Mathayo 24:36).  Atakuja haraka kama vile umeme utokavyo mashariki hadi magharibi (Mathayo 24:27). Atakuja wakati tusiotarajia kama mwizi anavyokuja usiku (2Petro 3:10). Siku hio itawajia kwa ghafla, kama mtego unasavyo (Luka 21:34). Bwana, katika hekima isiyo na vikomo, atarudi kumlipa kila mtu sawasawa na alivyotenda (Ufunuo 22:12). “Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, kesheni” (Marko 13:37).

Dalili za Nyakati na za Kurudi Kwake

Bwana ameeleza dalili ambazo kwazo tuweze kutambua kwamba kurudi kwake kumekaribia. “Basi, kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu: Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa u karibu, milangoni” (Mathayo 24:32-33). Kutakuweko:

  • Vita na matetesi ya vita (Mathayo 24:6)
  • Taifa litaondoka kupigana na taifa (Mathayo 24:7)
  • Matetemeko ya nchi, njaa na tauni (Mathayo 24:7)
  • Uovu utaongezeka, upendo utapoa (Mathayo 24:12)
  • Makristo na waalimu wa uongo (Mathayo 24:11, 24; Marko 13:22)
  • Siku kama wakati wa Nuhu (Mathayo 24:37)
  • Ishara katika jua, mwezi na nyota (Luka 21:25)
  • Mshangao wa mataifa na msukosuko (Luka 21:25)
  • Watu wakivunjika mioyo kwa hofu (Luka 21:26)
  • Watu wakisema amani na usalama (1Wathesalonike 5:3)
  • Nyakati za hatari (2Timotheo 3:1-5)
  • Wapendao anasa na wenye mfano wa utauwa (2Timotheo 3:1-7)
  • Watu waovu wakizidi kuwa waovu (2Timotheo 3:13)
  • Ukengeufu (Uasi) (2Wathesalonike 2:3)
  • Kujiweka akiba kwa ajili ya tamaa za kimwili (Yakobo 5:1-15)
  • Wenye kufanya dhihaka (2Petro 3:3-10)
  • Watu wenye kudhihaki wafuatao tamaa zao (Yuda 16, 17, 18)

Siku hizi asilimia kubwa ya dalili hizi zimedhihirishwa tayari. Uzinzi, uasherati, kuvunjika kwa ndoa na kuoana na mwingine, ushoga, uhalifu, na maovu yanaongezeka kwa haraka na kutapakaa kwa mapana. Hayo yote na dhambi zingine zinaharakisha kurudi kwa Bwana. Mambo haya yameandikwa “mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu” (2Petro 3:2). Watenda dhambi wataogopa kuona ujio wake, lakini watakatifu wataushangilia.

Maandiko kamili ya: Yesu Kristo Atakuja Tena

JE, UKO TAYARI? Unayo amani na Mungu na wanadamu wenzako? Je, kuna jambo lo lote katika maisha yako linalokuzuia kusema, “Amina; na uje, Bwana Yesu” (Ufunuo 22:20)?

 

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi