Udhuru - Je, Sasa Wewe ni Huru?

Tunaishi katika ulimwengu ambamo kila mmoja hupenda kutoa udhuru. Karibu kwa kila jambo linalogusa moyo wako hutaki kukubali au kuukabili ukweli jinsi ulivyo, kwa hiyo unatafuta njia ya kujitetea, ukidhania kwamba utetezi wako utakuweka huru. Je, unafikiri udhuru zako zitakuweka huru mbele za Mungu? Je, kuokolewa kunao udhuru? Visingizio ulivyo navyo kwa uhakika havitakuweka huru. Adamu na Hawa walipotenda dhambi, kila mmoja alijaribu kumwekea mwenzake lawama ya dhambi iliyotendeka, wakidhania kwamba Mungu angeachilia dhambi yao kwani wametoa sababu ni kwa nini waliingia dhambini. Lakini bado twasoma katika Biblia kwamba Mungu aliendelea kuwaadhibu tu. Mungu hazikubali udhuru zetu, hata zipangiwe kwa hila ya namna gani, au hata ukijifanya uonekane kuwa msafi kiasi gani. (Mwanzo 3:9-19; Wagalatia 6:7-8).

Wakristo waliorudi nyuma huwaga wanazitetea tabia zao na matendo yao yasiyo ya kikristo kwa kutoa visingizio. Unapoulizwa, “Kwa nini hukuwepo kanisani Jumapili iliyopita?” jibu lako litakuwa “Nilienda mahali”, au “Hili na hilo lilinibana, sikuweza kuhudhuria”. Unapokataa kuukubali ulegevu wako, inayofuatia ni VISINGIZIO- kwa njia zako za hila. Pamoja na maneno yako ya kujitetea, hujui kuwa mbele ya Mungu wewe ni kipofu, mwovu, uchi, maskini na fukara; na ole wao wasemao uovu ni wema na wema ni uovu. Eti unapoulizwa unaendeleaje katika maisha yako, unajibu ni njema. Wakati wewe siye mtu mwema, unajaribu kuficha hali halisi. Wakati ambao hutaki kuyasikiliza maonyo na ushauri juu ya maisha yako, unawaambia wanaokushauri, “Ni kwema tu kwangu”, ili wasiendelee kukusumbua zaidi. Mungu anakujua kabisa. (Isaya 5:20-21; Ufunuo 3:17; Waebrania 4:12-13)

Umwambiapo tajiri habari za Yesu, yaani Bwana na Muumba wake, yeye atakujibu kwa neno la kujisingizia, au atasema, “Sina muda sasa; Njoo, wakati mwingine utakaonifaa”. Kwa nini? Kwa sababu unapenda pesa, ndiyo maana ya kusema, “Siyo kwa sasa.” Maskini naye atasema, “Ni wenye fedha ndio wanaoweza kumtumikia Mungu vizuri. Sidhani nitaweza hadi hapo nitakapopata hela za kwangu”. Ninyi mfuatao pesa, ninyi matajiri msio na muda kwa Neno la Mungu, sawa basi, Mungu anawauliza swali: “Kwani itafaidiwa mtu nini akiupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” (Mathayo 16:26). “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi” (1Timotheo 6:6-10). Unaitafuta fedha kiasi kwamba unaacha kumsikiliza Mungu na kufanya mapenzi yake ambaye ni Muumba wako, uzima wako, aliye chanzo cha vyote kwako. (Luka 12:18-21)

Kuna visingizio vingi ambavyo watu hutoa kwa ajili ya hili na lile. Unapomwuliza rafiki yako au mwenye kuhudhuria kanisa, “Je, kwa nini hutaki kutoa maisha yako kwa Kristo? Kwa nini usitubu?” Baadhi ya maneno yao ya kujitetea ni haya: “Baba yangu ni Mwislamu. Hatakubali niwe Mkristo; Wazazi wangu wanavyo vyeo vya juu katika dini yao, na hili litakuwa doa katika sifa zao; Mama atanigombeza nikifanya hivyo; Kabla sijamaliza elimu yangu, sidhani kama nitaweza kuchagua kufuata njia nyembamba. Elimu ndiyo lengo langu la kwanza, na baada ya hapo, ndipo Mungu anafuata; Hadi hapo nitakapomwona msichana wa kuoa au mpaka hapo nitakapokuwa nimeolewa, siwezi kumtumikia Mungu vizuri; Mpaka nipate kazi au biashara yangu mwenyewe, sitaridhika kumtumikia Mungu. Nitakapopata kuendesha shughuli zangu vizuri ndipo baadaye nitamfikiria Mungu”. O Mwanadamu! O Mwanadamu! Hivyo ndivyo unavyomwambia Mungu, Muumba wako anayeshikilia pumzi ya uhai wako. Je, itakuwaje leo Mungu akikuambia, “Hutaweza kuona kesho”??? (Yakobo 4:14-17; Ezekieli 18:20; Mathayo 10:33-39; Luka 12:20; 14:18-20).

Maandiko kamili ya: Udhuru - Je, Sasa Wewe ni Huru?

Wokovu hauna visingizio. Ukweli ni kwamba hutaki KUJIKANA mwenyewe ili uepuke mambo ya dunia. Mungu anapokuambia utubu, hakuna udhuru kwa hilo. Unaweza kutubu SASA. Ukweli ni kwamba kuna maovu unayoyafanya na hutaki kuyaacha wala watu kuyajua, na pia hupendi kumfungulia Kristo moyo wako ili upate utakaso- kuoshwa na mambo uyapendayo zaidi ya Mungu. Unapenda elimu yako, umaarufu, cheo, sifa, baba, mama, mke, mume, hela, nk. zaidi ya Mungu. Sasa simama; ufikirie kwa muda baada ya kujiuliza maswali yafuatayo: “Je, ninafanya vizuri kwa kumkataa Mungu, nikitoa udhuru dhidi ya Roho Mtakatifu kila ajapo kuniita? Je, itakuwaje ikiwa nafasi hii ndiyo ya mwisho kwangu, na visingizio vyangu vitasababisha fursa hii inipitilize na kutoweka bila kujaliwa? Je, nitatoa nini badala ya nafsi yangu?”

Msomaji mpendwa, ni lazima ukubali ukweli huu kwamba siku moja Mungu atakuulizia maana ya kutokuwa mtiifu, halafu hutaweza kutoa utetezi tena! Hoo!! Ufunuo utakuwa wa namna gani! Hakuna kitakachofichwa siku hiyo! Swali la Mungu litachoma kiburi chote na kila udhuru kama moto ulao. Nabii Isaya, katika sura ya 30, mstari wa 1 asema: “Ole wao watoto waasi; asema Bwana; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi”. Je, si ni kiburi chako kinachokuzuia usijikabili nafsi yako jinsi ulivyo? Daima unajaribu kujitukuza na kukwepa aibu! Hutaki kukubali jinsi ulivyonajisika.

Katika siku ya mwisho, ule udhuru unaokuzuia usipate wokovu leo, utasimama dhidi yako na kukupinga. Rafiki zako uliofurahi nao watakuacha na watakabili hali yao wenyewe; ni wewe, ndiwe mwenyewe pekee yako, utaachwa na matendo yako. Ndiyo, na visingizio vyako vitakuwepo pale, lakini sasa vitakupinga, na utamkabili Mungu wewe mwenyewe pamoja navyo. Mungu atakapokuuliza, “Je, umefanyia nini wokovu niliokupa bure? Je, muda niliokuachia wa kutubu, uliufanyia nini ili upate wokovu wa bure?” Ndipo utaelewa kwamba maneno ya kujitetea uliyokuwa ukiyatoa yatashuhudia maangamizi yako ya kutisha. Utakuwa umechelewa mno kubadilika na kufanya mapenzi ya Bwana, na kitakachofuatia ni kutupwa katika shimo la moto lisilo na mwisho wake, penye majonzi, uchungu, na mateso daima kwa milele (Ufunuo 20:10).

Unajua udhuru zako zote. Jambo lile linalokuzuia usifanye mapenzi ya Bwana, limo moyoni mwako. Je, utaliruhusu jambo hilo likuzuie usiingie mbinguni? Pia, visingizio vyako sasa vitakupinga siku hiyo usiende mbinguni- kwamba una dhambi hii na ile moyoni mwako, na hivyo basi huwezi kuingia. Ndipo utagundua kwamba ulichokisema hapa duniani ili uwekwe huru, ndicho kitakachokufunga milele usifurahie utukufu wa Mbinguni.

Muda wa kutubu ni SASA- haujamalizika. Hata sasa Mungu anakuita wakati muda bado. Unaitwa leo, siyo kesho. “Uje nyumbani, maskini mwenye dhambi, mbona wapotea?” Mwokozi wako anaita, “Uje nyumbani”. Bwana alisema, “Njooni sasa, natusemezane pamoja, asema Bwana: Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu (Isaya 1:18). Ikiwa utakuwa mnyoofu wa kusikitikia dhambi na kufanya sala ya toba, usikawie, ondoa visingizio vyako na ufungue moyo wako wazi kwa Bwana. Usijifanye kuwa mwenye haki tena katika njia zako za uovu. Ikiwa utamwendea Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, yeye atakupokea—ukija kama mwenye dhambi ambaye hana utetezi.

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi