Masaa Arobaini na Nane Katika Jehanamu

Imeandikwa na John Reynolds

Mojawapo ya mifano iliyohai na ya kuvutia kabisa ya kurudishiwa uhai wa mtu aliyekwisha kufa ambayo imewahi kuja kwa ufahamu wangu ulikuwa ni ule wa George Lennox, mwizi stadi wa farasi kutoka Jimbo la Jefferson (Marekani). Alikuwa akitumikia kifungo chake cha pili. Jimbo la Sedwick lilimpeleka gerezani kwa mara ya kwanza kwa kosa hilo hilo – wizi wa farasi. 

Wakati wa majira ya baridi ya mwaka 1887 na 1888 alifanya kazi kwenye machimbo ya makaa ya mawe. Mahali alipokuwa akifanyia kazi palionekana kwake kuwa ni pa hatari. Hivyo, alitoa taarifa ya jambo hili kwa ofisa aliyehusika, ambaye alifanya uchunguzi, na baada ya kuamua kuwa chumba hicho kilikuwa ni salama alimwamuru Lennox arudi kwenye kazi yake. Basi mfungwa, akitii, alikuwa hajafanya kazi yake kwa zaidi ya saa moja, wakati sakafu ya juu ikaanguka chini ghafla na kumzika kabisa. Alibakia katika hali hii kwa masaa mawili kamili.

Alipokosekana wakati wa chakula cha mchana, msako ulifanywa kwa ajili ya mfungwa huyu, na alipatikana chini ya kifusi hiki cha udongo. Uhai ulionekana umemtoka. Alipelekwa hadi juu, na baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari wa jela, alitangazwa kwamba alikuwa ameshafariki. Mabaki yake yalichukuliwa hadi hospitalini ambapo alioshwa na kuvishwa, kabla ya mazishi. Jeneza lake lilitengenezwa na kuletwa hospitalini. Mchungaji wa gereza alikuwa amefika kuendesha ibada ya mwisho ya kuhuzunisha kabla ya mazishi. Wafungwa wawili waliamriwa na msimamizi wa hospitali kuinua marehemu kutoka kwenye mbao na kumbeba, kwa kupita katikati ya chumba na kuiweka ndani ya jeneza. Walitii, mmoja akishika kichwani na mwingine miguuni na walikuwa karibu kufika katikati ya chumba, wakati yule ambaye alikuwa kichani alijikwaa kwa bahati mbaya kwenye chungu cha maua, akayumba, na kudondosha maiti. Kichwa cha marehemu kilijigonga kwenye sakafu, na kwa mshangao mkubwa na wa kustaajabisha kwa wote waliokuwepo, sauti kubwa ya mlio wa maumivu ilisikika. Mara macho yalifumbuka na dalili nyingine za uhai zilijionyesha. Daktari aliitwa mara moja, na baada ya kufika, kama dakika thelathini, mtu aliyekufa alikuwa ameomba kikombe cha maji, na alikuwa katika tendo la kunywa wakati daktari alipowasili. Jeneza liliondolewa mara moja na lilitumika baadaye kumzikia mfungwa mwingine. Nguo zake alizovalishwa kwa ajili ya mazishi zilichukuliwa pia kutoka kwake na kuvalishwa badala yake vazi maalum la gereza. Katika kumfanyia uchunguzi alionekana kuwa mguu wake mmoja ulikuwa umvunjika katika sehemu mbili, na vinginevyo ulichubuliwa. Alibakia hospitalini kama miezi sita, na akarudia tena kufanya kazi.

Nilijifunza kuhusu hali yake ya ajabu aliyopitia wakati akiwa amekufa muda mfupi tu baada ya hapo, kutoka kwa mchimba makaa mwenzake. Nikisukumwa kwa udadisi, nilitamani kukutana na Lennox ili nisikie hali yake aliyopitia kutoka mdomoni mwake; nafasi hii ilikosekana kwa miezi  mingi. Hatimaye ilikuja. Baada ya kutolewa kutoka kwenye machimbo ya makaa ya mawe nilipangiwa kwenye mojawapo ya ofisi ya jela kutayarisha baadhi ya taarifa za mwaka. Suala la mtu huyu kufufuka tena lilikuwa likizungumzwa siku moja, akiwa akipita karibu na mlango wa ofisi na alionyeshwa kwangu. Haikuchukua muda hadi nilipompa karatasi kidogo mkononi mwake ya kumwomba aje mahali nilipokuwa nikifanya kazi. Alikuja, na hapo nilifahamiana naye vizuri, na kutoka midomoni mwake mwenyewe nilipata habari zake za ajabu. Yeye ni kijana, hawezi kuzidi umri wa miaka thelathini. Alikuwa ni mhalifu mzoefu; na alikuwa na elimu nzuri sana na hivyo mwenye akili sana.

Sehemu ya kustaajabisha kabisa ya habari zake zilikuwa ni ule wakati alipokuwa amekufa. Nikiwa mwanandishi wa habari, nilichukua habari zake kutokana na maneno yake.

Maandiko kamili ya: Masaa Arobaini na Nane Katika Jehanamu

Alisema; “Asubuhi yote nilikuwa na hofu ya kuwa jambo fulani la kutisha lingetokea. Sikujisikia vizuri katika hali yangu kiasi kwamba nilimwendea mkubwa wangu wa machimbo ya makaa, Bwana Grason, na kumwambia jinsi nilivyojisikia, na kumwomba aje na kufanya uchunguzi wa chumba changu cha makaa, mahali ambapo nilikuwa nikichimba makaa ya mawe. Alikuja  na alionekana kufanya uchunguzi thabiti, na aliniamuru kurudi, akisema hapakuwa na hatari na kwamba alidhani nilikuwa nikirukwa na akili! Nilirudi kazini kwangu, na nilikuwa katika kuchimbua kwa kadri ya saa moja, wakati ghafla ilikuwa giza kabisa, kisha ikaonekana kwamba lango kubwa  la chuma lilijifungua na nilipita katikati yake. Baadaye wazo lilinijia akilini mwangu kwamba nilikuwa nimekufa na niko katika ulimwengu mwingine. Sikuweza kumwona  mtu yeyote wala kusikia sauti ya aina yoyote. Kutokana na sababu ambayo mimi mwenyewe sikuifahamu, nilianza kuondoka kutoka kwenye lile lango wazi, na nilikuwa nimesafiri umbali fulani wakati nilipofika kwenye kingo za mto mpana. Haikuwa giza wala hapakuwepo na nuru. Kulikuwepo na mwangaza wa kutosha kama ilivyo katika usiku ulioangazwa kwa nyota. Nilikuwa sijabakia kwenye kingo za mto huu kwa muda mrefu wakati niliposikia sauti ya makasia ya mtumbwi majini, na mara mtu akiwa mtumbwini, akipiga makasia kuelekea mahali nilipokuwa nikisimama.

“Sikuweza kuzungumza neno. Aliniangalia kwa kitambo, na kisha alisema kwamba alikuwa amenijia mimi, na aliniambia kuingia mtumbwini na kuvuka hadi upande mwingine. Nilitii. Sikusema hata neno moja. Nilitamani kumwuliza kuwa yeye ni nani, na nilikuwa wapi. Ulimi wangu ulionekana kung’ania kwenye sehemu ya juu ya kinywa changu. Hivyo sikuweza kusema neno. Hatimaye, tulifikia ng’ambo ya pili. Nilitoka nje ya mtumbwi, na mpiga makasia ya mtumbwi alitoweka ghafla mbele ya macho yangu!

“Hivyo, nikiwa nimeachwa peke yangu, sikujua nifanye nini. Nikiangalia mbele yangu, niliona barabara mbili ambazo ziliongoza hadi kwenye bonde lenye giza. Mojawapo ya hizi, ilikuwa ni barabara pana na ilionekana kuwa inapitika sana. Nyingine ilikuwa ni njia nyembamba na ilielekea upande mwingine. Bila ya kufahamu, nilifuata barabara pana iliyokanyagwa sana. Nilikuwa sijaenda mbali wakati kulipoongezeka kuwa giza zaidi. Lakini kila baada ya muda, nuru iliweza kuangaza kutoka kwa mbali, na kwa jinsi hii niliweza kuendelea katika safari yangu.

 “Punde kidogo nililakiwa na kiumbe ambacho ni vigumu kabisa kwangu kukielezea. Ninaweza tu kukupa picha hafifu ya sura yake ya kuogofya. Alifanana na mtu kwa kiasi fulani, lakini alikuwa mkubwa zaidi kuliko mwanadamu yeyote ambaye niliwahi kumwona. Alikuwa siyo chini ya mita tatu kwa urefu wa kwenda juu. Alikuwa na mabawa makubwa mgongoni mwake. Alikuwa ni mweusi kama mkaa niliokuwa nikichimba, na alikuwa katika hali ya uchi kabisa. Alikuwa na mkuki mkononi mwake, ambao mpini wake ni lazima ulikuwa mita tano kwa urefu. Macho yake yaliwaka kama goroli za moto. Meno yake, meupe kama lulu, yalionekana kuwa inchi moja kwa urefu. Pua yake (ikiwa unaweza kuiita pua), ilikuwa kubwa sana, pana na bapa. Nywele zake zilikuwa ni za singa, nzito na ndefu. Zilitua juu ya mabega yake makubwa. Sauti yake ilisikika zaidi kama ngurumo za simba aliyeko kwenye zizi la wanyama kuliko kitu chochote ninachoweza kukikumbuka.

“Ilikuwa ni katika mmojawapo wa mimuliko hii ya nuru iliyoniangazia njia kwamba nilimwona kwa mara ya kwanza. Nilitetemeka kama jani nilipomwona. Alikuwa amenyanyua mkuki wake kama alitaka kunirushia. Ghafla nilisimama. Kwa sauti ile ya kutisha alinisihi nimfuate. Nikamwandama. Ningefanya jambo gani jingine? Baada ya kuwa amekwenda umbali fulani mlima mkubwa ulionekana kuinuka  mbele yetu. Sehemu iliyo mbele yetu ilionekana kusimama wima, kama vile mlima ulikuwa umekatwa katikati, na sehemu moja ilikuwa imechukuliwa. Juu ya ukuta huu uliosimama wima niliweza kuona kwa wazi kabisa maneno haya ‘Hii ni Jehanamu!’. Kiongozi wangu aliukaribia ukuta huu wima, na kwa mpini wake wa mkuki aligonga kwa sauti mara tatu. Lango kubwa tena zito lilifunguka na tuliingia ndani. Kisha niliongozwa kupita katika ile ambayo ilionekana kama ni njia ya ndani kwa ndani katika mlima huu.

“Kwa muda kadhaa tulisafiri katika giza nene. Niliweza kusikia vishindo vizito vya miguu ya kiongozi wangu na hivyo kuweza kumfuata. Katika njia yote niliweza kusikia sauti za mikoromo mizito kama ile ya mtu anayekufa. Mbele zaidi, mikoromo hii iliongezeka, na niliweza kusikia kwa wazi kabisa vilio vya ‘maji, maji, maji.’ Nikija sasa kwenye lango jingine, na kulipitia, niliweza kusikia mamilioni ya sauti kwa mbali, na mwito ulikuwa ni ‘MAJI.’ Punde kidogo lango jingine kubwa lilifunguka kutokana na kugonga kwa kiongozi wangu, na nilitambua kwamba tulikuwa tumekwisha pita ndani ya mlima, na sasa uwanda mpana ulikuwa mbele yetu.

 “Kwa mahali hapa kiongozi wangu aliniacha kwenda kuongoza roho zingine zilizopotea kuja mahali hapa. Nilibakia kwenye uwanda huu ulio wazi kwa muda, wakati kiumbe kilichofanana na kile cha kwanza kiliponijia; ila badala ya mkuki alikuwa na upanga mkubwa. Alikuja kuniambia kuhusu hukumu yangu ya baadaye. Alizungumza kwa sauti ambayo ilileta kitisho rohoni mwangu. ‘Uko katika Jehanamu’, alisema: ‘kwako wewe matumaini yote yametoweka. Ulipopita ndani ya mlima ukiwa njiani kuja hapa, ulisikia mikoromo na sauti zikilia kutokana na maumivu ya wale waliopotea walipokuwa wakiomba maji ya kupoza ndimi zao zilizokauka. Katika njia hiyo ndani ya mlima kuna mlango ambao unafungukia kwenye ziwa la moto. Muda sio mrefu hilo ndilo litakuwa hukumu yako. Kabla hujaongozwa hadi mahali hapo pa mateso ambapo hakuna kutoka tena – kwa kuwa hakuna tumaini kwa ajili ya wale ambao wameingia humo – utaruhusiwa kubakia kwenye uwanda huu wazi, ambako wapotevu wote wanapewa muda kwa kuangalia kile ambacho wangefurahia badala ya kile ambacho watateswa nacho.’

“Kwa maneno hayo, niliachwa peke yangu. Sijui kama ilikuwa ni matokeo ya hofu kubwa ambayo nilikuwa nimepitia, lakini sasa nilishikwa na bumbuazi. Hali ya kuishiwa kabisa nguvu iliushika mwili wangu. Nguvu yangu iliniacha. Miguu yangu haikuweza tena kuvumilia uzito wa mwili wangu. Nikiwa nimechoka kabisa, nilinyong’onyea hadi chini nikiwa bila ya msaada. Hali ya usingizi sasa ilinishika. Nusu nikiwa macho, na nusu nimelala, nikawa kama naota ndoto. Juu yangu kabisa na kwa mbali niliuona mji mzuri ambao tunausoma habari zake katika Biblia.  Uzuri wa ajabu kiasi gani jinsi kuta zake za yaspi zilivyokuwa. Niliona mbuga kubwa zilizofunikwa kwa maua zikijitandaza kila upande na kuenea mbali kabisa. Niliona pia mto wa uzima na bahari ya kioo. Makundi makubwa ya malaika waliweza kuingia na kutokea kwenye milango ya mji, wakiimba, eh, nyimbo nzuri kabisa. Kati yao nilimwona mpendwa mama yangu, ambaye alikuwa amekufa miaka michache iliyopita kutokana na kuvunjika moyo, kwa sababu ya uovu wangu. Aliangalia upande wangu na alionekana kuniita kwa kunipungia mkono wake. Lakini sikuweza kuondoka. Ilionekana kuna uzito mkubwa juu yangu mimi ambao ulinikandamiza chini. Sasa upepo mzuri ulipeperusha harufu nzuri ya maua yale ya kupendeza kuelekea kwangu, na niliweza sasa kwa wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kusikia wimbo mtamu wa sauti za malaika, na nilisema, eh, laiti ningeweza kuwa mojawapo!

“Nilipokuwa nakunywa kutoka kwenye kikombe hiki cha furaha, ghafla kiliondolewa kwa nguvu kutoka kwenye mdomo wangu. Niliamshwa kutoka kwenye usingizi wangu. Nilirudishwa kutoka kwenye nchi ya furaha niliyokuwa naota na mkaaji wa maskani yangu ya giza, ambaye alisema kwamba wakati ulikuwa umewadia wa kuingia kwenye makao yangu ya baadae. Aliniamuru nimfuate. Nikirudia nyuma niliingia tena kwenye njia ya giza ndani ya mlima na kumfuata kiongozi kwa kitambo, hadi tulipofika kwenye mlango ambao ulifungukia ubavuni mwa njia hii, na nikipitia kwenye mlango huu, tulijikuta hatimaye tunapita kwenye mlango mwingine, na Lo! Niliona Ziwa la Moto.

“Mbele yangu niliweza kuona, kwa kadri ya upeo wa jicho, lile ziwa halisi la moto na kiberiti. Mawimbi makubwa ya moto yaliweza kuvingirika moja juu ya jingine, na mawimbi mengine makubwa ya miali ya moto yakigongana na kuruka juu hewani kama mawimbi ya bahari wakati wa dhoruba kali sana. Kwenye vilele vya mawimbi niliweza kuona binadamu wakinywanyuliwa juu, lakini punde kidogo wakimezwa tena chini hadi kwenye vina vya chini kabisa vya ziwa hili la moto linalotisha. Wakati wakining’inia, kwa muda, juu ya vilele vya mawimbi haya makubwa yatishayo, makufuru yao dhidi ya Mungu wa haki yalikuwa ni ya kutisha, na vilio vya kuhuzunisha kwa ajili ya kuombaomba maji vikawa ni vya kuvunja moyo. Eneo hili kubwa la moto lilisikiwa tena na tena na vilio vya roho hizo zilizopotea.

“Punde kidogo niligeuzwa macho yangu kuelekea kwenye mlango ambao dakika chache kabla niliingilia, na nilisoma maneno haya ya kutisha, ‘Hii ndio hukumu yako; Milele haina mwisho’ Muda kidogo nilianza kuona ardhi ikididimia chini ya miguu yangu, na punde nilijikuta nazama chini kwenye ziwa la moto. Kiu isiyoelezeka kwa ajili ya maji ilinishika sasa. Na nikiitisha maji, macho yangu yalifumbukia kwenye hospitali ya jela.

“Sijawahi hapo nyuma kusimulia hali yangu hii niliyopitia kwa kuogopa kwamba wakuu wa gereza wangeisikia, wangenifikiria mimi ni mwenda wazimu na kunifungia kwenye nyumba ya vichaa. Nilipitia katika hali hii yote, na nimeshawishika kabisa kadri niishivyo hivi kwamba kuna Mbinguni na kuna Jehanamu, Jehanamu ya halisi, aina ile ambayo Biblia huzungumzia. Laki kuna jambo moja la hakika: kamwe siendi mahali pale tena.

“Mara nilipofungua macho yangu hospitalini na kuona kwamba nilikuwa hai na niko duniani kwa mara nyingine, mara moja nilimtolea Mungu moyo wangu na nitaishi na kufa kama Mkristo. Ijapokuwa picha za kuogofya za Jehanamu haziwezi kuondolewa kutoka kwenye kumbukumbu yangu, lakini pia mambo mazuri ya Mbinguni niliyoona siwezi kuyasahau. Nitakwenda kukutana na mpendwa mama yangu baada ya muda. Kuruhusiwa kuketi juu ya kingo za mto ule mzuri, kuzunguka pamoja na wale malaika kati ya mbuga, kupitia kwenye mabonde na juu ya vilima vilivyofunikwa kwa maua yenye harufu tamu, ambao uzuri wake unapita kitu chochote ambacho mwanadamu anaweza kuwazia, kusikiliza nyimbo za waliokombolewa-- hii yote itafidia kwa kuishi kwangu maisha ya Mkristo hapa duniani, hata ingawa nitapaswa kuziacha anasa nyingi za kimwili ambazo nilishirikia kabla ya kuja gerezani. Nimewaacha rafiki zangu nilioshiriki nao katika vitendo vibaya, na nitashirikiana na watu wema wakati nikiwa mtu huru tena.”

Tunatoa maelezo hayo kwa msomaji jinsi tulivyoyapokea kutoka kwa Lennox.

Mungu abariki ujumbe huu kutoka kwa Lennox kwa ajili ya kuzishtua roho nyingine nyingi zilizopotea. Eh, watu wanawezaje kutia shaka ya uwepo wa Jehanamu halisi inayowaka? Tunao Biblia, ambayo ni Neno la Mungu, pamoja na funuo za ajabu kama ya Bwana Lennox, ambazo zote zinafundisha kuhusu Jehanamu isio hadhithi tu. Wanaume  na Wanawake, acha! Ebu ukabili hali halisi! Maisha yako yameandikwa. Mungu anataka kukuokoa na atakusamehe ukiwa tayari kuungama kuwa wewe ni mwenye dhambi. Njia pekee ya wokovu ni kutakaswa kutoka dhambi, kwa kukubali kwamba damu ya Yesu imekuwa sadaka kwa ajili ya dhambi zako. Utakapokubali na msamaha huo wa Mungu, atakupa amani na raha moyoni mwako. Unaweza kuwa huru—huru hapa duniani, na zaidi, utakuwa huru kufurahia fahari za Mbinguni badala ya kuona sio tu masaa arobaini na nane, bali milele katika Jehanamu.

Soma na Luka 16:19-31

Kwa ajili ya Kutolewa Bure – Sio Kuuzwa

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Je, Ninaweza Kuokolewa? Nifanye Nini?

Hili ni swali zuri sana ambalo kila mmoja anapaswa kujiuliza. Biblia inaongelea njia kuu mbili tu; njia ya kwenda Mbinguni na njia ya kwenda Jehanamu. Mbinguni ni sehemu yenye kila kitu kizuri, na ni makao ya Mungu. Jehanamu ni mahali pa dhambi na maharibifu yasiyo na mwisho. Ni sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya Shetani na watoto wake. Je,nifanye nini ili niweze kufika mahali ambapo ni nyumbani mwa Mungu? Kama wewe si mkristo sahihi, na haujazaliwa kwa mara ya pili, basi unahitaji wokovu.

Maana ya kuokoka au kuzaliwa upya ni nini? Inamaanisha kupewa moyo mpya ambao unapenda kufanya yale Mungu aliyoyasema (Ezekieli 36:24-27). Inamaanisha kuacha yale matendo na maneno yote maovu pamoja na mawazo yetu maovu, na kumruhusu Yesu atuonyeshe yale tunayopaswa kuyafanya ili tumpendeze. Ina maana tumruhusu Yesu atuoshee dhambi zetu zote na kufanya mioyo yetu kuwa safi ili isiwepo dhambi itakayotutenga na Mungu(Matendo 3:19). Inamaanisha kubadilishwa kuwa mtu mpya ambaye hupenda kufanya yale tu yaliyo mema machoni pa Mungu, kama Moses alivyochagua kumfuata Mungu, na kama Mariam alivyopenda kuketi miguuni pa Yesu akisikiliza maneno yake (Waebrania 11:25; Luka 10:42).

Je, ni nani anayepaswa kuokoka? Kila mwanaume na kila mwanamke, kila mvulana na kila msichana ambaye ana umri wa kumwezesha kutambua mema na mabaya, mtu yeyote ambaye amefanya lisilo jema, yaani WOTE wanahitaji kupata wokovu. Isaya alisema, “Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe” (Isaya 53:6). Kila mmoja amefanya maovu ambayo hayampendezi Mungu, na hayo maovu yamefunika uso wetu kiasi kwamba hatuwezi kumwona Mungu (Isaya 59:2). Sasa lazima tufanywe kuwa watu wapya. Yesu aliweka dhahiri sana ukweli huu kwa Nikodemu, ambaye alikuwa mwalimu wa Israeli, Yesu alipomwambia, “Amin, amin , nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3-8). Yesu alimwambia Nikodemu ya kuwa ni kuzaliwa kiroho, na Roho Mtakatifu ndio atafanya hilo litokee. Hatuwezi kuona kitendo hicho kwa macho kama mtoto mdogo anapozaliwa, ila tunaweza kujisikia kikitokea, kama vile tunavyoweza kuhisi upepo kwenye uso wetu.

Yesu anatuambia leo, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30). Dhambi inakuwa kama mzigo mzito kwa mtu, wakati anapofikiri kuhusu kukutana na kifo na hukumu ya makosa yake. Yesu anatusihi tumpelekee kila dhambi tuliyo nayo maishani mwetu, na tuzishushe zote miguuni pake. Yesu anataka “tupokee upatanisho”(Warumi 5:11) na tuwe huru na mizigo yetu mizito. Yesu ameteswa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, na alimwaga damu yake, na alikufa msalabani kama dhabihu “kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote”(1Yohana 2:2). Ni lazima tuwe tayari kuona ya kwamba tumetenda dhambi, na lazima tutambue ya kwamba tuna hatia. Halafu inabidi tuamini ya kuwa Yesu aliteswa na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na ametulipia gharama ya dhambi zetu. Kwenye Mithali twasoma, “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa: bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”(Mithali 28:13).

Maandiko kamili ya: Je, Ninaweza Kuokolewa? Nifanye Nini?

Kuna tumaini kwako hata kama wewe ni mwenye dhambi mkubwa. Bwana anasema, ”Haya njoni tusemezane. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18). Ijapokuwa dhambi zetu ni nyeusi kama usiku, Yesu anataka kuzisafisha ziwe nyeupe kama nguo mpya. Mungu anatusihi tumwendee na dhambi zetu zote na kuzungumza naye juu ya hizo dhambi. Halafu Yesu anataka kutusafisha hizo dhambi kwenye damu yake, ili tuwe na “wale walioshinda kwenye dhiki kuu na kuosha mavazi yao na kuyafanya meupe kwa damu ya mwanakondoo” (Ufunuo 7:14). Huyo mwanakondoo ni Yesu Kristo ambaye alimwaga damu yake pale msalabani kwa ajili yetu.

Biblia inatuambia ya kwamba kila mmoja wetu, wanaume kwa wanawake, wavulana kwa wasichana, tumekuwa mwenye dhambi na tumepoteza utukufu wa Mungu (Warumi 3:23). Lakini Mungu hatuachi bila tumaini, kwa kuwa Mungu anamuamuru kila mmoja kila mahali atubu (Matendo 17:30). Tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe dhambi zetu na atatusafisha njia zetu mbaya (1Yohana 1:9). Ikiwa tumemwudhi ama tumemkosea mtu, ama tukimwibia kitu ama kumdanganya, ama tumesema uongo ama tukifanya kitu kingine chochote ambacho ni dhambi, lazima tuzungumze na huyo tuliyemtendea mabaya, pamoja na Mungu, na kuwaambia hali halisi. Kama tumechukua kitu ambacho si chetu ni lazima tumrudishie au tumlipe gharama yake, au kuweka sawa kwa namna nyingine na yule tuliyemwibia. Luka anatusimulia hadithi ya Zakayo. Zakayo alikuwa tayari kurudisha mara nne ya mali alizochukua ambazo hazikuwa halali yake(Luka 19:1-10). Lazima tuhuzunike moyoni kwa sababu ya dhambi zetu, na tuwe tayari kurekebisha matendo maovu, kama Zakayo alivyofanya. Pia inatupasa kufanya amani na wale tuliowakosea. Hii ndio kumrudia Bwana wetu Yesu kwa moyo wako wote, na roho yako yote, na akili zako zote, na nguvu zako zote (Marko 12:30).

Lazima tuamini mioyoni mwetu kwamba Mungu alimfufua Yesu kwenye mauti, na kwamba Yesu yupo hai leo. Wakati tunaamini hili, basi inabidi tukiri ya kuwa Yesu ni Bwana wetu na Mwokozi. Kama tutaungama dhambi zetu zote na tutamwamini Yesu Kristo na moyo wetu wote na nguvu, na tukimkiri kwa mdomo wetu, basi tutaokolewa (Warumi 10:9). Yesu amesema anasimama mlangoni akibisha hodi. Mtu yeyote akiisikia sauti yake, na kuufungua mlango, ataingia moyoni mwake, na atafanya moyo huo makao yake (Ufunuo 3:20). Yesu anasema atakaa na mtu huyo maadamu huyo mtu yuko tayari kumtii Mungu. Eh ni utamu kiasi gani kujua Yesu! Amechukua dhambi zetu zote, na tunayo “amani iliyokamilika kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1).

Kila mmoja aliyepata msamaha wa dhambi, na amani ya Mungu ni kiumbe kipya kwa sababu hafanyi maovu aliyokuwa anafanya awali. Mambo ya kale yote yamekwisha na anaishi maisha mapya na Mungu. Kila kitu ni kipya kwa sababu Mungu anamwongoza huyo mtu, na Mungu anamwambia jinsi ya kuishi (2Wakorintho 5:17). Hajisikii lawama tena, na habebi mzigo mzito wa dhambi kila wakati kwa maana anatembea na Roho wa Mungu (Warumi 8:1). Mambo ambayo macho yanapenda kutazama, na mwili huu wa duniani unapenda kufanya, na kiburi cha maovu kinachotoka kwa Shetani, na maovu mengine yote tunayosoma katika Wagalatia, HAYAPO kwenye maisha ya mtu huyo tena (Wagalatia 5:19-21; 1Yohana 2:15-17). Yeye ni kiumbe kipya na anafurahia matunda yote ya Roho Mtakatifu ambayo tunayasoma katika Wagalatia. Anajua kuwa anayo ahadi “ya maisha ya sasa, na yale yajayo” (1Timotheo 4:8; Wagalatia 5:22-25). Mtu huyo sasa ni Mkristo mwenye furaha sana aliyeokoka, na anao uhakika ya kwamba yeye ni mtoto wa Mungu.

Baada ya kuzaliwa upya, na kupata amani hii na Mungu, ni lazima uendelee kutembea kwa “ujasiri katika fundisho la Mitume” kama vile Mitume wa Yesu walivyofanya (Matendo 2:42). Ni lazima uwe makini kufanya yale Yesu aliyokuambia kufanya, na usimruhusu Shetani akusukume pembeni ya njia ilionyooka tena. Usimwache Shetani akuibie amani ya Mungu tena. Uwe makini sana Shetani asije akakushawishi kurudia tena yale maovu ambayo yalikuwa ni mzigo mzito uliolemewa nao awali. Ongea na Mungu kila siku, na umwombe Mungu akuongoze njia ya mbinguni ambako hakutakuwa na dhiki wala mateso, bali amani na furaha milele (Ufunuo 21:1-7).

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Maisha Yako Yameandikwa

Biblia hutuambia kwamba Mungu anajua kila kitu, na kwamba anahifadhi maandishi ya maisha yetu. Tutahitajika kutoa maelezo ya aliyoandika siku ya hukumu (Warumi 14:11-12). “Na niliwaona wafu, wadogo kwa wakubwa wamesimama mbele ya Mungu; na vitabu vilifunguliwa: na kitabu kingine cha uzima kikafunguliwa, na wafu walihukumiwa kwa yale yaliyoandikwa katika vitabu kulingana na kazi zao” (Ufunuo 20:12).  Tutakaposimama katika hukumu mbele ya Mungu, tutakuwa tumechelewa kubadili maisha yetu wala mwisho wetu wa milele.

Mungu huona yote, mema na maovu tunayoyafanya. Yeye hufahamu msimamo wetu halisi na mawazo yetu--- ikiwa mema au maovu. “Wala hakuna kiumbe chochote kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote ni utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu” (Waebrania 4:13). Tutahukumiwa kwa orodha ya matendo yetu. “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya” (Mhubiri 12:14).

CHAGUO NI LETU

Katika uhai huu tunaweza kuchagua kumfuata Kristo na mafundisho yake au kufuata tamaa ya mwili wetu unaopenda dhambi. Biblia ina orodha ya dhambi za mwili katika Wagalatia sura ya 5. Ndiyo haya, “Uasherati, uzinzi, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, ugomvi,wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo” (Wagalatia 5: 19-21). Ikiwa baadhi ya haya yamepatikana kwetu, andiko hili hutuambia kwamba hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Kwa neema ya Baba wa Mbinguni aliye na upendo, tukitubu na kumwamini Kristo, tunapata msamaha. Kisha damu ya Kristo hufunika dhambi na zinafutwa kwenye orodha.

Pia Biblia inayo orodha ya matunda yanayozalishwa katika maisha yetu tunapojitoa kwa Mungu. “Lakini matunda ya roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utulivu, wema, imani, upole, kiasi…..” (Wagalatia 5:22-23). Ni muujiza wa neema kuwa na matunda haya pamoja na majina yetu kuandikwa Mbinguni.

Maandiko kamili ya: Maisha Yako Yameandikwa

Neno la Mungu hutuonya juu ya mtego na hatari ambayo inatukabili. “Pia jueni hili, kwamba katika siku za mwisho nyakati za hatari zitatokea. Kwa maana watu watajipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu, wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao” (2Tim 3:15). Ni dhahiri kwamba hali zilizo katika ulimwengu hazifai maisha ya ukristo. Tumezungukwa na uovu wa kila namna ya ulaghai. Kwa kuwa tunawajibika kwa kila neno na tendo letu, tunapaswa kufanya chaguzi ambazo zitazalisha matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu.

Katika Biblia kuna mafungu mengi yanayotuonya kuhusu kutokujali wokovu wetu. “Na kama wenye haki hawaokolewi, Je, watakuwaje wenye dhambi na wasiomcha Mungu?” (1Petro 4:18).  “Na Bwana alimwambia Musa, yeyote anitendaye dhambi, nitafuta jina lake katika kitabu changu” (Kutoka 32:33). “Njooni mmtazame mtu (Yesu) aliyeniambia yote niliyoyatenda” (Yohana 4:29). Ingawa maneno haya ni yenye uzito Mungu ameahidi kutusamehe dhambi kama tumeamini na kutubu katika damu ya Kristo ya kulipia deni. Atazifuta dhambi zetu badala ya kufuta majina yetu kutoka kwenye orodha.

JE, JINA LAKO LIPO KATIKA KITABU CHA UZIMA?

Ili majina yetu yaandikwe katika kitabu cha uzima, ni lazima tuukubali mwaliko wa Yesu: “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao, na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28). Hakuna anayesamehewa hatia ya dhambi pasipo damu ya Yesu. Yeye kwa sababu ya upendo, alimwaga damu yake kwa hiari juu ya msalaba kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu alimwambia Nikodemo, “Mtu asipozaliwa kwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3). Pia alisema, “Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 18:3). Yesu huwaalika kila mmoja kuja kwake na kuokolewa.

Baada ya majina yetu kuandikwa katika kitabu cha uzima tusitake yafutwe tena. Yesu asema, “Tazama, naja upesi: Shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako” (Ufunuo 3:11). Na tena, “Kesheni mkiomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41). Maandiko haya yanatuonya kuwa wanaokesha na siyo kuacha ahadi yetu ya kumtumikia Mungu. Shetani, adui wa nafsi zetu, ameelezwa kama simba angurumae, ambaye ataturarua tusipompinga kwa kuwa imara kwenye imani. (1Petro 5:8-9) Tunapaswa kulichunguza Neno la Mungu na kuwa thabiti katika sala zetu, la sivyo wokovu wetu utatuteleza. Tumeahidiwa, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, na sitaondoa jina lake katika kitabu cha uzima, lakini nitakiri jina lake mbele ya Baba yangu, na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).

KUWA TAYARI KWA SIKU YA HUKUMU

Leo ndiyo siku ya neema, ni nafasi ya kutengeneza nyumba yetu na kujiandaa kwa siku ya hukumu. Tukifa miili yetu inayokufa itarudi mavumbini. Lakini atakaporudi Yesu kuuhukumu ulimwengu siku ya ufufuo, kila mmoja atapokea mwili usiokufa ambao utakaa milele mbinguni au motoni. Kama kuna doa la dhambi mioyoni mwetu, tumgeukie Yesu LEO aisafishe, kisha twaweza kuwa tayari kuingia mbinguni siku hiyo kuu. “Na hakitaingia mle kilicho najisi, wala afanyaye machukizo, wala mwongo: bali wale walioandikiwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” (Ufunuo 21:27).

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi