Je, Ninaweza Kuokolewa? Nifanye Nini?

Hili ni swali zuri sana ambalo kila mmoja anapaswa kujiuliza. Biblia inaongelea njia kuu mbili tu; njia ya kwenda Mbinguni na njia ya kwenda Jehanamu. Mbinguni ni sehemu yenye kila kitu kizuri, na ni makao ya Mungu. Jehanamu ni mahali pa dhambi na maharibifu yasiyo na mwisho. Ni sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya Shetani na watoto wake. Je,nifanye nini ili niweze kufika mahali ambapo ni nyumbani mwa Mungu? Kama wewe si mkristo sahihi, na haujazaliwa kwa mara ya pili, basi unahitaji wokovu.

Maana ya kuokoka au kuzaliwa upya ni nini? Inamaanisha kupewa moyo mpya ambao unapenda kufanya yale Mungu aliyoyasema (Ezekieli 36:24-27). Inamaanisha kuacha yale matendo na maneno yote maovu pamoja na mawazo yetu maovu, na kumruhusu Yesu atuonyeshe yale tunayopaswa kuyafanya ili tumpendeze. Ina maana tumruhusu Yesu atuoshee dhambi zetu zote na kufanya mioyo yetu kuwa safi ili isiwepo dhambi itakayotutenga na Mungu(Matendo 3:19). Inamaanisha kubadilishwa kuwa mtu mpya ambaye hupenda kufanya yale tu yaliyo mema machoni pa Mungu, kama Moses alivyochagua kumfuata Mungu, na kama Mariam alivyopenda kuketi miguuni pa Yesu akisikiliza maneno yake (Waebrania 11:25; Luka 10:42).

Je, ni nani anayepaswa kuokoka? Kila mwanaume na kila mwanamke, kila mvulana na kila msichana ambaye ana umri wa kumwezesha kutambua mema na mabaya, mtu yeyote ambaye amefanya lisilo jema, yaani WOTE wanahitaji kupata wokovu. Isaya alisema, “Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe” (Isaya 53:6). Kila mmoja amefanya maovu ambayo hayampendezi Mungu, na hayo maovu yamefunika uso wetu kiasi kwamba hatuwezi kumwona Mungu (Isaya 59:2). Sasa lazima tufanywe kuwa watu wapya. Yesu aliweka dhahiri sana ukweli huu kwa Nikodemu, ambaye alikuwa mwalimu wa Israeli, Yesu alipomwambia, “Amin, amin , nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3-8). Yesu alimwambia Nikodemu ya kuwa ni kuzaliwa kiroho, na Roho Mtakatifu ndio atafanya hilo litokee. Hatuwezi kuona kitendo hicho kwa macho kama mtoto mdogo anapozaliwa, ila tunaweza kujisikia kikitokea, kama vile tunavyoweza kuhisi upepo kwenye uso wetu.

Yesu anatuambia leo, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30). Dhambi inakuwa kama mzigo mzito kwa mtu, wakati anapofikiri kuhusu kukutana na kifo na hukumu ya makosa yake. Yesu anatusihi tumpelekee kila dhambi tuliyo nayo maishani mwetu, na tuzishushe zote miguuni pake. Yesu anataka “tupokee upatanisho”(Warumi 5:11) na tuwe huru na mizigo yetu mizito. Yesu ameteswa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, na alimwaga damu yake, na alikufa msalabani kama dhabihu “kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote”(1Yohana 2:2). Ni lazima tuwe tayari kuona ya kwamba tumetenda dhambi, na lazima tutambue ya kwamba tuna hatia. Halafu inabidi tuamini ya kuwa Yesu aliteswa na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na ametulipia gharama ya dhambi zetu. Kwenye Mithali twasoma, “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa: bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”(Mithali 28:13).

Maandiko kamili ya: Je, Ninaweza Kuokolewa? Nifanye Nini?

Kuna tumaini kwako hata kama wewe ni mwenye dhambi mkubwa. Bwana anasema, ”Haya njoni tusemezane. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18). Ijapokuwa dhambi zetu ni nyeusi kama usiku, Yesu anataka kuzisafisha ziwe nyeupe kama nguo mpya. Mungu anatusihi tumwendee na dhambi zetu zote na kuzungumza naye juu ya hizo dhambi. Halafu Yesu anataka kutusafisha hizo dhambi kwenye damu yake, ili tuwe na “wale walioshinda kwenye dhiki kuu na kuosha mavazi yao na kuyafanya meupe kwa damu ya mwanakondoo” (Ufunuo 7:14). Huyo mwanakondoo ni Yesu Kristo ambaye alimwaga damu yake pale msalabani kwa ajili yetu.

Biblia inatuambia ya kwamba kila mmoja wetu, wanaume kwa wanawake, wavulana kwa wasichana, tumekuwa mwenye dhambi na tumepoteza utukufu wa Mungu (Warumi 3:23). Lakini Mungu hatuachi bila tumaini, kwa kuwa Mungu anamuamuru kila mmoja kila mahali atubu (Matendo 17:30). Tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe dhambi zetu na atatusafisha njia zetu mbaya (1Yohana 1:9). Ikiwa tumemwudhi ama tumemkosea mtu, ama tukimwibia kitu ama kumdanganya, ama tumesema uongo ama tukifanya kitu kingine chochote ambacho ni dhambi, lazima tuzungumze na huyo tuliyemtendea mabaya, pamoja na Mungu, na kuwaambia hali halisi. Kama tumechukua kitu ambacho si chetu ni lazima tumrudishie au tumlipe gharama yake, au kuweka sawa kwa namna nyingine na yule tuliyemwibia. Luka anatusimulia hadithi ya Zakayo. Zakayo alikuwa tayari kurudisha mara nne ya mali alizochukua ambazo hazikuwa halali yake(Luka 19:1-10). Lazima tuhuzunike moyoni kwa sababu ya dhambi zetu, na tuwe tayari kurekebisha matendo maovu, kama Zakayo alivyofanya. Pia inatupasa kufanya amani na wale tuliowakosea. Hii ndio kumrudia Bwana wetu Yesu kwa moyo wako wote, na roho yako yote, na akili zako zote, na nguvu zako zote (Marko 12:30).

Lazima tuamini mioyoni mwetu kwamba Mungu alimfufua Yesu kwenye mauti, na kwamba Yesu yupo hai leo. Wakati tunaamini hili, basi inabidi tukiri ya kuwa Yesu ni Bwana wetu na Mwokozi. Kama tutaungama dhambi zetu zote na tutamwamini Yesu Kristo na moyo wetu wote na nguvu, na tukimkiri kwa mdomo wetu, basi tutaokolewa (Warumi 10:9). Yesu amesema anasimama mlangoni akibisha hodi. Mtu yeyote akiisikia sauti yake, na kuufungua mlango, ataingia moyoni mwake, na atafanya moyo huo makao yake (Ufunuo 3:20). Yesu anasema atakaa na mtu huyo maadamu huyo mtu yuko tayari kumtii Mungu. Eh ni utamu kiasi gani kujua Yesu! Amechukua dhambi zetu zote, na tunayo “amani iliyokamilika kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1).

Kila mmoja aliyepata msamaha wa dhambi, na amani ya Mungu ni kiumbe kipya kwa sababu hafanyi maovu aliyokuwa anafanya awali. Mambo ya kale yote yamekwisha na anaishi maisha mapya na Mungu. Kila kitu ni kipya kwa sababu Mungu anamwongoza huyo mtu, na Mungu anamwambia jinsi ya kuishi (2Wakorintho 5:17). Hajisikii lawama tena, na habebi mzigo mzito wa dhambi kila wakati kwa maana anatembea na Roho wa Mungu (Warumi 8:1). Mambo ambayo macho yanapenda kutazama, na mwili huu wa duniani unapenda kufanya, na kiburi cha maovu kinachotoka kwa Shetani, na maovu mengine yote tunayosoma katika Wagalatia, HAYAPO kwenye maisha ya mtu huyo tena (Wagalatia 5:19-21; 1Yohana 2:15-17). Yeye ni kiumbe kipya na anafurahia matunda yote ya Roho Mtakatifu ambayo tunayasoma katika Wagalatia. Anajua kuwa anayo ahadi “ya maisha ya sasa, na yale yajayo” (1Timotheo 4:8; Wagalatia 5:22-25). Mtu huyo sasa ni Mkristo mwenye furaha sana aliyeokoka, na anao uhakika ya kwamba yeye ni mtoto wa Mungu.

Baada ya kuzaliwa upya, na kupata amani hii na Mungu, ni lazima uendelee kutembea kwa “ujasiri katika fundisho la Mitume” kama vile Mitume wa Yesu walivyofanya (Matendo 2:42). Ni lazima uwe makini kufanya yale Yesu aliyokuambia kufanya, na usimruhusu Shetani akusukume pembeni ya njia ilionyooka tena. Usimwache Shetani akuibie amani ya Mungu tena. Uwe makini sana Shetani asije akakushawishi kurudia tena yale maovu ambayo yalikuwa ni mzigo mzito uliolemewa nao awali. Ongea na Mungu kila siku, na umwombe Mungu akuongoze njia ya mbinguni ambako hakutakuwa na dhiki wala mateso, bali amani na furaha milele (Ufunuo 21:1-7).

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Je, ni Vipi Kuhusu Madawa ya Kulevya, Pombe, na Uzinzi?

Tukabili hali halisi. Maovu ya kutisha - pombe, madawa ya kulevya, na zinaa - vinatishia na kuharibu kile kilichoubwa na Mungu kuwa kizuri. Vinakamata na kuwavuta wadogo kwa wakubwa kama mikono ya pweza mkubwa inavyoshika.

Maambukizo kwa jamii ya leo ni makadirio makubwa. Watu wengi wamelegea bila nanga na kuachwa na laana ya pombe, madawa ya kulevya, na zinaa, wakielekea maangamizi ya milele. Watu wanavutwa upesi na wenzao, pamoja na matangazo yanayotolewa na video, radio, na magazeti kuhusu maovu hayo. Akili inashambuliwa mpaka inachanganyakiwa na kukaa na mawazo ya machafuko ambayo matokeo yake ni uharibifu wa kiroho na kimwili.

Je, akina nani walaumiwe kwa nidhamu na mwenendo wa kuaibisha wa namna hii? Je, ni vijana? Siyo lazima. Kwa kutokumcha Mungu, maisha ya wazazi yamewaidhinishia dhambi ambazo kizazi cha vijana kinapenda. Akina baba na mama hawajui kwamba wanawafundisha watoto wao tabia mbaya ya madawa na ulevi kwa kushindwa kujizuia wenyewe. Kanuni za maadili ya Mungu zimeachwa kwa kutokujali. Kilio cha nguvu kingepanda juu mbinguni. Je, jinsi gani tujiokoe sisi na watoto wetu?

Miji yetu, shule zetu, na vyuo vyetu haziwezi kuzalisha raia katika kiwango kinachofaa kwa mataifa yetu ikiwa matumizi ya dawa za kulevya na pombe huvumiliwa na kuhimizwa kwa uzembe wa wazazi na waalimu.

Matumizi ya pombe ni uharibifu mkubwa wa maadili ya taifa, yakiharibu maamuzi, sifa, na maisha kwa ujumla. Huchangia kuvunjika na kugawanyika kwa familia, ambayo ni mojawapo baraka za Mungu kwa ajili ya wanadamu.

Maandiko kamili ya: Je, ni Vipi Kuhusu Madawa ya Kulevya, Pombe, na Uzinzi?

Zaidi, kuna ongezeko la matumizi ya madawa haramu. Madhara mabaya ya madawa haya ya kulevya ni makubwa zaidi ya faida yao.Utumiaji wa madawa ya kulevya inaweza kusababisha uharibifu wa akili. Watumiaji wa dawa za kulevya wanakubali kwamba hio ni mtego wa mauti: kiakili, kimwili, na kiroho. Uharibifu wa ubongo usiotibika, mauaji, na kujiua ni matokeo mabaya ya anasa hizi.

Kwa sababu ya tabia zao za asili kwa kutamani dhambi, watu wako tayari kufuata mwelekeo na tamaa zinazobuniwa na Shetani. Katika hali hii mwili unataka kuridhishwa pasipo kuzuiliwa. Zinaa hauzimi moto wa tama, bali inachochea. Kuzini siyo uponyaji kwa tamaa, kama vile pombe siyo tiba ya ulevi. Ukweli ni kwamba, tunapaswa kukabili tamaa zetu. Tamaa zinatokea miili yetu ambao itaishia hapa hapa duniani tutakapokufa. Nafsi zetu, yenye kudumu milele, inatamani kuheshimu amri za Mungu.

Uzinzi, Uasherati, Ushoga, Usagaji, na kujamiana na wanyama kumekatazwa na Neno la Mungu. (Walawi 18:23; Wagalatia 5:19-21). Uzinzi huleta maumivu, huzuni, maangamizi, hatia, na magonjwa ya zinaa. Usafi huleta busara ya kujistahifu na heshima. Tusidhani kwamba mtu anayetimiza tamaa zake ndiye mwenye uhuru wala mwenye furaha---hii ni uongo mkubwa. Atendaye dhambi ndiye mtumwa wa dhambi. Mwenye uhuru ndiye anayejikana na kutii sheria ya Mungu.

Wakati watu wametumbukia katika ziwa hilo la tope la ufisadi na upofu wa kiroho, na kuwa na ujasiri wa kutomcha Mungu, Biblia Takatifu imekwisha kujenga msingi ya nidhamu na haki. Bila shaka Biblia ndiyo yenye mamlaka ya milele juu ya masuala ya mema na mabaya. Mungu alimuumba binadamu na haja ya ngono kwa uzazi wa mataifa na kuimarisha au kuboresha kifungo cha ndoa kati ya mume na mke. Aliidhinisha kutimiza haja hii ndani ya ndoa iliyo halali tu. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. (Waebrania 13:4).

Mtume Paulo anaandika katika kitabu cha Warumi kuhusu hukumu ya Mungu juu ya kujamiana kijinsia moja (Ushoga/Usagaji). Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa, ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti; wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. (Warumi 1:26-28,32). Hii ilikuwa ni dhambi ya Sodoma na Gomora iliyochukiza, na Mungu aliwaletea hukumu. (Mwanzo 19). Kulingana na maandiko ni haiwezekani kuwa na Roho Mtakatifu mioyoni mwetu wala kuishi maisha ya Mkristo ikiwa twafanya dhambi hizi.

 Msomaji mpendwa, ili uwe na furaha halisi katika maisha, ili uwe na amani na Mungu, unapaswa kuwa na uhusiano naye. Tambua kwamba wewe ni mwenye dhambi na uungame, na uamini kwamba Yesu alikufa msalabani  akichukua lawama yako. Ushindi unakusubiri!

Unapomfungulia Mungu moyo wako na kuziungama dhambi zako, atakusamehe. Tukizungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote. (1 Johana 1:9)

Kwa hiari mkabidhi Yesu maisha yako yote kama Mwokozi wako, na ufuate Neno lake pamoja na Roho Mtakatifu kwa utiifu kweli kweli. Baraka zinazopatikana katika maisha  yaliyobadilika ni fikira safi zinazoleta mabadiliko ya ajabu katika matendo yetu na kazi zetu. Kristo atakupa ushujaa kukabili matatizo ya maisha na atakupa nguvu kushindia majaribu ambayo yaweza kukushambulia. Njoo kwa Yesu sasa wakati akikuita. Mtafuteni Bwana madamu anapatikana, mwiteni  madamu yu karibu. (Isaya 55.6)

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Nguvu Za Giza

Kutambua Mbinu za Shetani kwa Kutumia Mwanga wa Neno la Mungu.

Lengo la Biblia Takatifu silo kuangalia hasa Shetani na kazi zake. Japokuwa tunapata mengi kwenye Biblia yanayofunua tabia zake na kazi zake.

Wakati fulani Shetani alikuwa malaika, lakini aligeuka kinyume cha Mungu, Muumba wake, na akatamani kuwa kama Mungu. Matendo ya ufalme wa giza wa Shetani siyo mageni. Yanaonyesha dhahiri jitihada za Shetani kwa miaka kupingana na Ufalme wa Mungu. Anatoa mbadala wa kile ambacho Mungu anatimiliza kwa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu.

Twasoma katika kitabu cha Kutoka juu ya nguvu ya walozi wa Misri waliojaribu kufanya miujiza Mungu aliyofanya kwa mkono wa Musa. Na kwenye kitabu cha Ayubu, Shetani anadhihirishwa kama mwenye wivu sana juu ya uaminifu wa Ayubu kwake Mungu. Alitumia ukatili na unyang’anyi ili ajaribu kumlazimisha Ayubu kwenda kinyume na Mungu.

Njia za shetani zinatambuliwa na: Woga, vitisho, ahadi za kupata anasa na nguvu, misukumo, mashaka, na tuhuma. Baadhi ya mambo ya kwanza anayoyatambulisha kwetu yanaonekana ni ya kuvutia sana na ya kusisimua. Anashauri, “Ungependa kujua mambo ya mbeleni au kuwa na ufahamu ambao wengine hawawezi kuwa nao?” Anaweza kukupa uponyaji ambao uko nje ya idara ya kisayansi. Utabiri wa mambo yajayo huenda unaonekana kwamba hauna madhara wala ubaya, lakini unafuatwa na mengine ya uchawi wa macho, pamoja na kutumia dawa za kienyeji na uchawi wa kumroga mtu, na hatimaye kumpelekea mautini. Wazo linaanza kutuingilia kuwa kuna baadhi ya roho za kuheshimiwa na kuogopwa kwa sababu ya nguvu zilizo nazo juu yetu. Kwa hiyo, Shetani anawanasa hao wasiokuwa waangalifu kwenye mtego wake wa kuendeshwa na woga kwake na roho zake.

Watu wengi sana wamekamatwa na shauku ya vitu ambavyo, kwa mara ya kwanza vilionekana kuwa vyema. Kwa kufanya majaribio ya utabiri wa mambo yajayo na uchawi wa aina mbalimbali, watu wanajiweka kwenye mazingira hatarishi ya kusumbuliwa zaidi na mapepo ya giza.

Lengo la shetani ni kumomonyoa na hatimaye kuharibu imani ya mkristo kwa Mungu. Mkristo apata ushindi kwa kuwa na imani kwa Yesu Kristo peke yake. Wakati mwingine hamu ya kujua visivyojulikana au matamanio ya nguvu vinamsukuma mtu afanye majaribio na hayo ambayo ni ya ufalme wa Shetani. Imani ya kukaza kwa Mungu humpumzisha mtu asivutiwe na yale yasiyojulikana na pia inamimarisha kabisa katika nguvu za Kristo.

Maandiko kamili ya: Nguvu Za Giza

Yale yaliyoanza kutokana na shauku au majaribio punde yanamnasa mtu kwenye wavu wa hofu, hofu ya kile kinachoweza kutokea mbeleni, hofu ya nguvu kuu, hofu ya watu wengine, hofu ya Shetani mwenyewe. Hizi hofu zinamfunga mtu aliyeruhusu mwenyewe kujihusisha na matendo yasiyo na uhakika. Kutibu hofu hii, Shetani anadai kuwa anao dawa nzuri: Eti atatoa nguvu zaidi kama mtu atajisalimishia utaratibu fulani au kutii amri kadhaa. Shetani asema kwamba hofu ya roho nyingine zinaweza zikashindwa kwa kujipatia nguvu kubwa zaidi kwetu wenyewe. Kwa hiyo mtu anaingizwa kwenye hatua za kufikia nguvu zaidi ambazo, badala ya kumpandisha kwenye kiwango cha juu cha amani, zinamzamisha chini katika kina kirefu cha machukizo ya kishetani. Usalama ulioahidiwa na shetani hauonekani, na hubadilishwa kwa uhitaji wa kulindwa na nguvu zilizo juu zaidi kwenye huu ufalme wa uovu. Huu ndio mfumo wa kishetani.

Mpango wa shetani ni kumzidi Mungu. Shetani aliumbwa kuabudu, na sio kuabudiwa. Yeye sio nguvu ya juu; hawezi kumzidi Mwana Kondoo wa Mungu; hawezi kutoa amani; hana nia na ushindi wetu. Hata hivyo anaendelea na kazi ya kuwatawala watu ili watu wamtumikie yeye. Anajaribu kuleta mashaka kuhusu Mungu na ufalme wake. Anajitahidi kuanzisha taasisi yake na yeye akiwa kama mfalme. Hii inaendelezwa kwa utaratibu wa hofu na udanganyifu wa nguvu. Anafanya miujiza ili awashangaze na kushawishi watu kusudi awawekee kifungo akilini mwao (2Wakorintho 11:14,15). Madhara ya mtego huu ni kuharibu amani na usalama kwa watu binafsi, majumbani, na hata serikalini. Hio inawakamata watu, na inasababisha wajisikie kutishwa sana kama watajaribu kutorokea ufalme huo.

Shetani ni mkali sana, mchoyo sana, mkatili sana, adui mbaya sana uliye naye wewe. Yeye hana heshima hata kidogo. Yeye ni mwongo. Hakuna ukweli ndani yake- “Yeye ni mwongo, na ni baba wa huo [uongo]” (Yohana 8:44). Yeye ni muuaji, mharibifu. Yeye ni mfano wa chuki na uovu. Yeye ni mwovu kabisa ambaye hana uzuri uliobakia kwake!

Shetani ni mchochezi wa maovu yote. Hakuna kosa wala dhambi ambayo kwake ni ovu sana au chafu sana kwake. Yeye ni chanzo cha chuki zote, mauaji yote, kila aina ya kutesa watoto au kupiga wanawake, kila aina ya madawa ya kulevya, kila aina ya uzinzi, ndoa zote zilizovunjika, kila aina ya kutokuelewana, kila uchawi, kila kutokuwa na uaminifu. Anafurahi kusababisha hamu ya kuvunja sheria na uovu, uvunjaji wa sheria unaofanyika juu ya watu wengine wema ambao, kwa bahati mbaya, wanaangukia mikononi mwa wasio haki na wapotovu. Yeye ni mkatili na hana msamaha. Hana huruma kwa hao wanaopata mateso. Kumwaga damu na vifo ndio silaha anazotumia kutekeleza kazi zake. Amekuja “kuiba, kuua, na kuharibu” (Yohana 10:10).

Mwisho wa milele wa Shetani ulishaamulika. Kuna sehemu ya moto wa milele ilishaandaliwa kwa ajili yake na malaika wake (Mathayo 25:41). Anajishughulisha na kupata watu wengi kadiri atakavyoweza ili wapate hayo mateso pamoja naye. Anajua anaweza kufanya hivi kwa kuimomonyosha, kuidhoofisha, na mwishowe kuiangamiza imani yetu kwa Mungu. Atafanya hivi kwa kulipinga Neno la Mungu kwa uwazi, ama kwa ujanja na werevu anawahamasisha “wakristo” walio vugu vugu, wasiojali, na waliokubali Ukristo usio na masharti.

Kuna ukombozi kutoka kwenye umiliki na utumwa wa Shetani. Atakufanya uamini ya kuwa hakuna njia ya kutoka. Biblia inatuambia ya kwamba Yesu alikuja kuwaweka huru waliotekwa mateka. Amekuja kuleta uzima. Yesu ni njia, kweli, na uzima (Yohana 14:6). Wakati alipokuwa hapa duniani, Yesu alionyesha nguvu zake juu ya Shetani kwa kushindana na majaribu ya Shetani na akitupa nje nguvu za giza kwa kutumia Neno la Mungu (Mathayo 4:1-11; Marko 9:25,26). Yesu alishinda nguvu za Shetani kwa kifo chake msalabani na kufufuka kwake kutoka wafu.

Je, tunawezaje kujumuishwa katika ushindi huo wa kumzidi huyu adui mkuu wa nafsi zetu? Kwanza, lazima tufahamu ya kwamba tulikuwa tumetekwa na shetani na kufungwa na hofu yake. Lazima tukubali kwamba huku ni hali ya dhambi na kwamba tumepotea tukibakia hali hii. Tunapogundua hili kwamba hatuwezi kujiokoa wenyewe kutoka mkononi mwa Shetani, lazima tumlilie Mungu ukombozi wake kwa moyo wetu wote. Lazima tuzitubu na kuziacha dhambi zetu. Twahitaji kukubali kwa imani, damu ya Yesu Kristo yenye utakaso kwa ajili ya dhambi zetu. Lazima tujitoe nafsi zetu kwa Mungu, kukubali msamaha wake na kwa uaminifu kutii Neno lake. Tunapotimiza haya masharti, anatupa amani kwake, anayatuliza mahangaiko mioyoni mwetu, anasamehe dhambi zetu, anatufanya kuwa kiumbe kipya na kutufanya mmoja wa wanawe. Hii ndio inamaanisha kuzaliwa upya. Yeyote anayepinga mwito wa Mungu bado yumo katika ufalme wa Shetani, na mwishowe, mdanganyi atampeleka huyo mtu pamoja naye kwenye mateso ya milele.

Kama huelewi mpango ambao Mungu amekuwekea, jifunze Neno la Mungu, na umwombe Yeye kwa uaminifu moyoni, na atakuonyesha njia. Mungu anakuita kwake na anataka wewe utoroke na utumwa wa Shetani. Mungu akubariki. Soma Zaburi 91.

Masomo Mengine:

Luka 11:20-23 Mmoja mwenye nguvu zaidi ya Shetani

Warumi 6:20-23 Kuwa huru kutoka kwenye dhambi

Isaya 61:1 Kuwekwa huru mateka

Warumi 8:1,2 Kuwa huru na laana na hatia

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi