Hamna Budi Kuzaliwa Mara ya Pili

Yesu anatuambia kwamba milango ya mbinguni imefungwa dhidi yetu isipokuwa tunazaliwa mara ya pili. Kwa hiyo twauliza: “Rafiki, umezaliwa mara ya pili?” “Muumini wa kanisa, umezaliwa mara ya pili?” Ikiwa hapana, basi umepotea. Kwa maana Yesu anasema, “Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3). Kwa kweli hakuna mtu anayetaka kufa akiwa mwenye dhambi, au kupotea; basi hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

Unaweza ukauliza, “Kuzaliwa mara ya pili maana yake ni nini?” Leo, kuna mafundisho mengi ya uongo kuhusu kuzaliwa mara ya pili. Siyo ubatizo, kwa kuwa wengine walibatizwa na bado hawajazaliwa mara ya pili (Matendo 8:9-25). Siyo kujiunga na kanisa, kwa sababu wengine waliingia ndani kwa siri bila kufahamika (Wagalatia 2:4). Siyo kula meza ya Bwana, kwa maana baadhi walikula isiyostahili na iliwaletea hukumu (1Wakorintho 11:29). Siyo kubadilika au kujaribu kuishi maisha bora, “kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze” (Luka 13:24). Siyo kusali, kwa maana Yesu asema, “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami” (Mathayo 15:8).

Mtu mwingine anaweza akasema, “Nikijaribu kuyafanya yote niwezayo: kuwapa maskini, kuwatembelea wagonjwa na kuwa mwema kila siku kadiri niwezavyo, basi kwa kweli nimezaliwa mara ya pili.” La, hasha, hatuwezi kuwa tofauti na jinsi tulivyo moyoni. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu wala haiwezi kuitii” (Warumi 8:7). “Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.” (Mathayo 7:18) Tunapaswa kuwa na moyo uliobadilika. Kwa kuwa Mungu kupitia manabii, asema hivi, “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” (Ezekieli 36:26).

Hivyo basi, kuzaliwa upya maana yake nini?” Kiini cha kuzaliwa upya ni kuwa na mabadiliko ya moyo kutoka kwa maisha ya kujitumikia kibinafsi, na kupata maisha ya kumtumikia Bwana. Mabadiliko haya hutokea wakati tunapojutia dhambi zetu, na kwa imani tukamtazamia Yesu kwa kuomba msamaha. Mtoto azaliwapo, uhai mpya unatokea, binadamu mpya katika mwili. Hali kadhalika, tunapozaliwa upya kwa roho, uhai mpya huu hutokea ambao ni ndani ya Yesu Kristo na unaongozwa na Roho Mtakatifu. Hivyo basi, kunaitwa kuzaliwa: uhai mpya ndani ya Kristo Yesu. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yaki, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba (2Petro 3:9).

Maandiko kamili ya: Hamna Budi Kuzaliwa Mara ya Pili

“Ni lini nitegemee kuzaliwa mara ya pili?” Maandiko matakatifu yasema, “Leo, kama mtaisikia sauti yake,” (Waebrania 3:7). Hii inamaanisha kwamba katika umri wowote, wakati wowote, au mahali popote, ukisikia mwito wake na kuitika unaweza ukazaliwa kwa mara ya pili kwa njia ya Roho.

“Itachukua muda gani? Si nitakua taratibu katika kuzaliwa upya?” La, tunazaliwa kwanza katika ufalme wa Mungu na kunatufanya tuwe wana na warithi. “na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo” (Warumi 8:17). Kuzaliwa mara ya pili kunaweza kutokea mara moja unapomtolea Yesu vyote na kumwendea kupata msamaha.

“Kwa njia gani na lini ninaweza kuupokea?” Mungu anayechunguza moyo, aona uaminifu wako. Anakujia kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu, na kuumbia moyoni mwako roho wa kweli. (Zaburi 51:10) Kwa njia hii unazaliwa upya- kiumbe kipya katika Kristo Yesu kwa kuwa na imani kwake. (2Wakorintho 5:17).

Hatimaye: “Kwa jinsi gani naweza kufahamu kwamba nimezaliwa upya tayari?” Paulo katika Warumi 8:1-10 anafundisha; “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo sio wake”. Biblia yafundisha kwamba waliopotea wamekufa dhambini, wamelaaniwa, na wana dhamiri iliyo ya uovu. Wana mawazo yenye tamaa ya kimwili, wasio na tumaini, wasiotii, na wasio na Mungu ulimwenguni. Lakini Mkristo aliyezaliwa mara ya pili ni mtoto wa Mungu, yu hai katika Kristo, ameokolewa, hana hatia ya dhambi, na anayo dhamiri safi. Naye anayo nia ya kiroho, amejazwa na Roho Mtakatifu na imani, na analo tumaini la uzima wa milele. Dhambi zake zimeondolewa kwa damu ya Yesu Kristo. Moyo wake umejazwa na upendo na amani wa Mungu zinazozidi ufahamu wote. Anayapenda mapenzi ya Bwana, na anayo shauku na amepewa uwezo kuyafanya mapenzi hayo. Pia anatembea na tumaini la uzima ng’ambo ya kaburi, na anayo ahadi ya makao yaliyopo mbinguni. Je, mtu anaweza kupata mageuzi kama haya na asiyatambue? La, hasha kwani “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:16). Ikiwa hujapata mabadiliko haya yaletayo amani na furaha moyoni, usipuuze, mtafute Mungu kwa moyo mmoja; kwa kuwa ni roho yako mwenyewe. Ni lazima uzaliwe mara ya pili.

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi